 Ras Ebrahim Makunja Yafuatayo ni mahojiano baina ya Kongoi Media Productions na mwanamuziki mahiri Ras Ebrahim Makunja toka Tanzania aishiye Ujerumani. Ras Ebrahim Makunja vile vile ni mwasisi wa bendi ya Ngoma Africa Band. Tunachapisha mahojiano haya kwa lugha ya Kiswahili. Ras Makunja, ni nini haswa madhumuni ya kuundwa kwa bendi ya Ngoma Africa? Ngoma Africa imeanzishwa kwa malengo ya kuutangaza muziki wa dansi wa Tanzania na miziki ya kiasili, nje ya Tanzania. Kuupa uhai muziki wa dansi wa Tanzania na kukieneza kiswahili kwa njia ya muziki. Kuitangaza Tanzania kwa mlingoti wa "muziki wa Dansi". Ngoma Africa ni mabalozi wa muziki wa dansi. Ngoma Africa huimba nyimbo nyingi katika lugha ya Kiswahili lakini pia inaimba nyimbo katika lugha mbali mbali za Afrika Mashariki.
Kwa maoni yako Ras Makunja, ni kwa nini muziki wa dansi wa Tanzania ulichelewa kufika kaatika majukwaa na masoko ya kimataifa kwa miaka mingi? Wanamuziki wakongwe wa Tanzania toka enzi hizo walijitahidi kufanya kazi kwa uhodari, na muziki wetu wa Tanzania ulikuwa unawika ndani ya Afrika Mashariki na Kati. Nyimbo kama DADA ASHA ya Tabora Jazz ilitingisha KINSHASA. Simba wa Nyika waliunguruma kila kona huko Kenya. Mbaraka Mwinshehe na Morogoro Jazz walitingisha Japan (1970). Marehemu Patrick Balisidya na Afro 70 walishea jukwaa moja na STEVE WONDER, katika maonyesho ya Lagos. Msondo Ngoma (baba wa Muziki) walikuwa Msumbiji katika sherehe za uhuru, 1975. Sikinde Ngoma ya Ukae walikuwa Zimbabwe, na wengi wengineo.
 The Ngoma Africa Band Wakongwe hao walijitahidi kutaka kuutoa muziki wa Tanzania nje ya TZ. Lakini kilichowakwamisha zaidi ni STUDIO. Tanzania wakati ule kulikuwa na studio moja tu ya RTD, na Serikari haikutilia maanani sana swala la sanaa na muziki. Fani hii lilichukuliwa kuwa ni STAREHE, na sio bidhaa inayoweza kuuzwa nje au kuitangaza Tanzania nje.
Baada ya Serikali kuanzisha bendi za mashirika ya Umma, wanamuziki wengi wakongwe ilibidi waajiliwe na mashirika ya Umma, na kuongozwa na mameneja wa bendi ambao hawakuwa wataalamu wa muziki. Mameneja walikuwa wakiamrisha wanamuziki. Mpango huu wa kuanzishwa bendi za mashirika ulichangia kuziua bendi kongwe Kama Dar-es-salaam Jazz, Tabora Jazz, Westen Jazz, Kiko Kids, Unyanyembe, Kilwa Jazz na kadhalika. Bendi moja tu ya shirika la wafanyakazi, NUTA Jazz (sasa Msondo Ngoma, Baba aw Muziki),ndio iliyoweza kuishi hadi leo; kutokana na bendi hiyo imejaa wataalam mahiri waliobobea katika fani hii ya muziki, na ndiyo bendi kongwe iliyobakia barani Afrika. Hata hizo bendi za mashirika ya Umma nazo zilikufa! Sio kwa kukosa vyombo bali manejmenti mbaya. Bendi kama UDA, URAFIKI, BIMA LEE, STC!
Kuhusu mashindano ya masoko kati ya muziki wa dansi na muziki wa kizazi kipya? Hakuna mashindano yoyote kati ya miziki hii kwani so called "Muziki wa Kizazi Kipya" ni mtindo wa Kupita na wa muda mfupi! Yaani nina maana wapenzi wa kizazi kipya baada ya miaka kumi ijayo watakuwa kizazi cha zamani!
Na kama muziki huu wa kizazi kipya hautakuwa na msingi imara wa "Roots" za muziki wa dansi, utakuwa ni sawa na nyumba ya matofali ya barafu, au mti usio na mizizi.
Muziki wa dansi hauna mshindani wala mpinzani, kwa miaka na miaka umekuwapo na mitindo mingi ya kigeni ilivamia Tanzania na bendi nyingi za kigeni nazo zilikuja na zikafa, lakini "muziki wa dansi" bado upo hai. Mfano, katika miaka ya 70, kulikuwa na bendi za kigeni kama Nova sucsses iliyokuwa inamilikiwa na Cosmas, Papa Micky(mkongo). Bendi kama Orch. Baba Gaston ya Baba Ilunga wa Ilunga, Orch.Nkashama Nkoy; zote zilikuja na kutoweka au kuyeyuka. Lakini bendi kongwe kama Msondo Ngoma, DDC Mlimani Park aka sikinde, Kilimanjaro Band (Njenje) bado zipo. kwa maana hii, huu ni ushaidi hai kwamba "Muziki wa dansi wa Tanzania" hauna mpinzani wa mshindani. Kinachotakiwa ni kasi ya kuutoa nje ya Tanzania na kufunika soko la kimataifa.
Wakati ule pia kulikuwa na bendi za kizazi kipya, kama Vile Tonics Band ya Michael Pangalala, Bigots Band, Sun Burst ya marehem Kassim Rajabu Magati, Barkeys; na nyingine nyingi ndogo ndogo zilikuwa zinapiga mitindo ya Pubping, Bug, walizozichanganya na vionjo vya Kitanzania. Hizo bendi nazo zilipita. Bendi za muziki wa dansi bado zipo! Marquis Du Zaire na Orch.OSS ziko wapi? Lakini DDC na Msondo ngoma bado zipo.
Sasa Ngoma Africa ipo, na msimamo wake wa kutangaza muziki wa dansi wa Tanzania. Hivyo na tunawaomba watanzania watuunge mkono ili tuitangaze asilimali yetu hii fahari ya kitanzania. Watuunge mkono kwa kuiporomoti bendi yao "The Ngoma Africa" kuitangaza Ngoma Africa. Kama vile kununua CD za Ngoma Africa, na Kuzipiga mara kwa mara radioni nyimbo za Ngoma Africa.
Una maoni gani au mtazamo gani kuhusu muziki wa kizazi kipya? Si jambo jema kuingilia kazi za wanamuziki wengine au kuwakosoa,lakini si dhambi kutoa maoni yangu, ili mradi simvunjii mtu heshima. Kufanya ni kuleta mapinduzi ya utamaduni ndani ya jamii, kwa kupeleka ujumbe wa RAP YA KISWAHILI ni vema! Pia shughuli yao hiyo imezalisha ajira nyingi. Lakini wanachotakiwa kufanya ni kuweka vionjo vyenye maadili ya utamaduni wa Tanzania. Wajaribu sana kusikiliza tyuni za wakongwe wa nyumbani na kujituma kwa kupiga na bendi badala ya kutegemea play back
Wajaraibu kuchukua muda sana wa kutupia jicho nyimbo au mashairi yao kabla ya kurekodi. Na wajaribu kuyafanya kuwa mafupi, yakiwa marefu mno yanapoteza maana na ujumbe. Wengi wao wameshaanza kupiga na bendi, ni vyema, lakini wasiogope kuwa karibu na wakongwe wa dansi maana watasoma mengi na watajikuta muziki wao sio Big G tena.
Ni nini mtazamo wa baadaye wa Ngoma Africa? The Ngoma Africa Band ni sawa na Taasisi ya Umma! Bendi hii ni daraja linalo unganisha Tanzania, Africa Mashariki na Ulaya. Kwa maana hii basi tungependa sana katika siku za baadaye kuona daraja hili, au taasisi hii inakuwa kuungo katika wanamuziki walio nyumbani na bendi ya Ngoma Africa,kwa maufaa ya pande zote mbili. Kazi hii ya ubalozi iwezwe kufanywa pia na walio nyumbani. Ni matumaini yetu pia walio nyumbani wataichukulia Ngoma Africa kuwa ni bendi yao, kwa kuweza kuipa kila nafasi.
Kwa nini Msondo Ngoma hawajakuja Ulaya! Mimi sio msemaji wa Msondo Ngoma! Ninawaheshimu sana. Lakini hili ni swala la Watanzania walio Ulaya kuwapa nafasi bendi za dansi zilizo nyumbani! Nitafurahi sana kuona bendi kongwe zinaletwa Ulaya. Sikinde walikuwa hapa Ujerumani mwaka 2007.
Wito wako kwa wanamuziki wa Tanzania? Wito wangu kwa wanamuziki wa Tanzania walio nyumbani na nje ya nyumbani, kwanza waondoe uwoga na wajiamini, yaani wasijione kuwa ni wanamuziki wa daraja la pili. Kwa maana hii basi, wanamuziki walio nyumbani lazima wajahamini kuwa MUZIKI WA TANZANIA UNAPENDWA KIMATAIFA na una nafasi kubwa ya kuweza kufunika soko la kimataifa. Hapa nina maana muziki wa dansi na miziki ya kiasili ina nafasi kubwa sana kimataifa. Lakini watanzania wenyewe lazima tuache tabia ya uwoga na kutokujiahami.
Pili, Wito wangu kwa wazalendo wezangu walio nje ni kwamba Watanzania walio nje ya nyumbani wasisite wala kuona haya kuwapendelea kwa kuwapa nafasi wanamuziki wa kitanzania, iwapo pale watakaposikia kuwa kuna nafasi au tamasha linahitaji wanamuziki au bendi basi watanzania walio nje wasifanye hajizi hata kidogo! Nafasi hiyo lazima watupe sisi watoto wao na wenzao kufanya hivyo haitakuwa ubaguzi bali UZALENDO. Kuhusu The Ngoma Africa Band: The Ngoma Africa band, "the Golden Voice Of East Africa" ni bendi ya asili ya Tanzania yenye makao yake nchini Ujerumani. Bendi hii ya The Ngoma Africa Band ilianzishwa 1993. Mwasisi wa bendi hiyo ni Ebrahim Makunja, Ras Makunja kwa jina la kisanii, ambaye pia ndio kiongozi, mtunzi na mwimbaji. Bendi hii ilianzishwa baada ya mafanikio ya utafiti wa miziki ya kiasili na makabila mbali mbali nchini Tanzania na nchi jirani za Afrika Mashariki.

Related items |